Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Urambo limekutana katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo tarehe 12.09.2024 kwa ajili ya kufanya mkutano wa mwaka, ambapo mkutano huo umepokea taarifa ya shughuli mbalimbali zilizotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Urambo katika kipindi cha mwezi Julai 2023 hadi Juni 2024.
Mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Mhe. Adam Malunkwi, umepokea taarifa hiyo kutoka kwa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo ambapo taarifa hiyo imegusa mapato na matumizi pamoja na mafanikio, changamoto na mikakati ya Halmashauri katika kutekeleza shughuli mbalimbali katika mwaka mpya wa fedha 2024/2025.
Akiwasilisha taarifa hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Bi. Grace Quintine amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo ililenga kukusanya kiasi cha Tsh. 3,076,270,000 kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato ya ndani. Hata hivyo hadi kufikia Juni 30, 2024 Halmashauri ya Wilaya ya Urambo ilifanikiwa kukusanya kiasi cha Tsh. 3,510,090,017.09 ambayo ni sawa na asilimia 114 (114%) hivyo kuvuka lengo la makusanyo katika Mwaka wa fedha 2023/2024.
Aidha Mkurugenzi Quintine amesema pamoja na changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Halmashauri katika mwaka wa fedha 2023/2024, Halmashauri ilipata mafanikio mbalimbali kupitia divisheni, idara pamoja na vitengo vyake ambapo ni pamoja na kufanikisha ujenzi na ukamilishaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, uboreshaji wa huduma mbalimbali n.k
Baada ya kuwasilishwa kwa taarifa hiyo wajumbe waliweza kupongeza kwa taarifa nzuri pamoja na kupongeza usimamizi bora wa shughuli za Halmashauri hasa katika ukusanyaji wa mapato kwani ni mara ya kwanza kwa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato ya ndani. hata hivyo wajumbe waliweza kupongeza mafanikio mengineyo ambayo Wilaya iliyafikia katika mwaka wa fedha 2023/2024 ikiwemo kushika nafasi ya kwanza Kitaifa katika Mbio za Mwenge wa uhuru wa Mwaka 2023.
Aidha, pamoja na kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Halmashauri, Mkutano huu ulifanya uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti pamoja na Wenyeviti wa kamati mbalimbali za Halmashauri ulioenda sambamba na uteuzi wa wajumbe wa kamati hizo kulingana na sheria na kanuni.
"Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, jitokeze kushiriki Uchaguzi"
Bomani Urambo
Anunani ya posta: Mkurugenzi Mtendaji (W), 30 Br ya Boma Stendi, S.L.P 170. 45582 Urambo Tabora
Simu ya mezani: +255 (0) 262 965 824
Simu ya mkononi: DED GRACE:0786821141
Barua pepe: ded@urambodc.go.tz
Copyright ©2025 Urambo . All rights reserved.