Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Bi. Grace Quintine amesema kinachopelekea Watoto wa Kike kutopenda kusoma masomo ya Sayansi ni kutokana na kukatishwa tamaa na watu wanaowazunguka.
Bi. Quintine amesema hayo wakati akifungua Semina ya siku mbili ya kuhamasisha Mtoto wa kike kupenda na kusoma masomo ya Sayansi Wilayani Urambo.
Kampeni hiyo inayohusisha Semina pamoja na ufuatiliaji wa matokeo inayofadhiliwa na Shirika la UNICEF imefanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Kitaifa ya Wasichana ya Margareth Sitta na kuhusisha Walimu Wakuu wa shule za Sekondari 17, Walimu wa masomo ya Sayansi, Viongozi wa Serikali za Vijiji na Vitongoji pamoja, Viongozi wa dini pamoja na wawakilishi wa wazazi.
Katika ufunguzi wa Semina hiyo Mkurugenzi Quintine amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amejikita katika kuweka usawa wa kijinsia katika nyanja mbalimbali, lakini pasipo na watoto wa kike wengi wenye elimu itakuwa ngumu kupata wanawake wa kufaa katika nafasi hizo. Hivyo amesisitiza kuwa Washiriki wa semina hiyo kuwa makini katika mafunzo watakayopewa ili wawe mabalozi wazuri wa kuhamasisha wazazi na watoto wa kike kusoma masomo ya Sayansi.
Aidha Bi. Grace Quintine amesema kuwa Mtoto wa Kike ana upeo mkubwa wa kiakili ambapo anaweza kusoma masomo hayo na kufaulu vyema kwani hata yeye alifaulu masomo hayo kwa kuyasoma kwa miezi kadhaa alipokuwa Sekondari, Hivyo amewaasa wawaelimishe wazazi kuepuka mawazo potofu ya kuwa mtoto wa kike hana manufaa kwa mzazi kwani mtoto wa kike ni rahisi zaidi kumhudumia mzazi wake pale anapopata uwezo wa kufanya hivyo.
Hata hivyo amesema jamii inapaswa kuepukana na Mila kandamizi kwa Mtoto wa kike kwani watoto wote wa kike na wakiume wana haki sawa.
Amehitimisha kwa kusema kuwa kumkatisha tamaa na kumuozesha mapema mtoto wa kike kabla hajatimiza ndoto zake ni kuharibu viongozi wa kesho watakaohudumia jamii, hivyo jamii inapaswa kuwapa moyo watoto wa kike kila mtu kwa nafasi yake ili kupata viongozi bora wajao.
Bomani Urambo
Anunani ya posta: Mkurugenzi Mtendaji (W), 30 Br ya Boma Stendi, S.L.P 170. 45582 Urambo Tabora
Simu ya mezani: +255 (0) 262 965 824
Simu ya mkononi: DED GRACE:0786821141
Barua pepe: ded@urambodc.go.tz
Copyright ©2024 Urambo . All rights reserved.