Timu ya Madaktari Bingwa wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeacha alama njema Wilayani Urambo kwa kutibu wagonjwa zaidi ya 250, kupitia Kambi waliyoiweka kwa muda wa Siku tano kuanzia tarehe 29.09.2025 hadi tarehe 03.10.2025.
Akizungumza katika hafla ya kuwaaga Madaktari hao, Mkuu wa Wilaya ya Urambo Mhe. Dkt. Khamis Mkanachi amewapa pongezi madaktari hao kwa kuitekeleza kazi yao vyema na kufanikisha kutoa huduma kwa Wananchi wa Urambo kama ilivyokusudiwa.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Bi. Grace Quintine ameungana na Mkuu wa Wilaya ya Urambo kwa kuwashukuru Madaktari hao na kueleza kuwa maoni yaliyowasilishwa na madaktari hao ameyapokea na yatakwenda kufanyiwa kazi ili kuboresha zaidi Hospitali ya Wilaya ya Urambo.
"Tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuletea Madaktari bingwa, kwani wanatoa huduna nzuri ambayo Wananchi wengi wasingeweza kuifikia kiurahisi, pia tunawashukuru kwa huduma waliyoitoa kwa wananchi na tunaamini wakati ujao wananchi wataendelea kujitokeza kwa wingi,
Kama Halmashauri tumepokea maoni mbalimbali kutoka kwa madaktari bingwa na tutayafanyia kazi ili tuweze kuleta ufanisi katika Hospitali yetu ya Wilaya ya Urambo" ameeleza Bi. Grace Quintine
Kwa niaba ya timu ya Madaktari Bingwa waliotoa huduma Wilayani Urambo, Dkt. Anastazia Komba (Daktari bingwa wa dawa za Usingizi na Ganzi - MOI) ameeleza kuwa wananchi wamekuwa na muitikio Mkubwa na wamefurahia huduma, pia wamepata ushirikiano Mkubwa kutoka kwa watumishi wa Hospitali ya Wilaya ya Urambo pamoja na Uongozi wa Wilaya kwa kuwa nao bega kwa bega tangu mwanzo wa utoaji wao wa huduma.
Aidha Dkt. Komba amemalizia kwa kusema kuwa Wananchi wa Wilaya ya Urambo na maeneo jirani wajitahidi kujitokeza kwa wingi zinapotokea fursa za Madaktari bingwa kwani huduma hizi hupatikana katika hospitali kubwa hapa nchini ambapo ni mbali na maeneo wanayoishi.
Sambamba na hilo Bw. Salum Hamis Mihambo Mkazi wa Kata ya Urambo ambaye ni mmoja kati ya Wananchi waliopata huduma za madaktari hao ameonyeshwa kufurahishwa na huduma yao huku akiwasisitiza Wananchi kutumia vyema nafasi kama hii.
Bomani Urambo
Anunani ya posta: Mkurugenzi Mtendaji (W), 30 Br ya Boma Stendi, S.L.P 170. 45582 Urambo Tabora
Simu ya mezani: +255 (0) 262 965 824
Simu ya mkononi: DED GRACE:0786821141
Barua pepe: ded@urambodc.go.tz
Copyright ©2025 Urambo . All rights reserved.