Urambo - Tabora
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Bw. Masudi I. Masudi amewapongeza na kuwashukuru wananchi wa kata ya Nsenda kwa kutoa eneo lenye ukubwa wa ekari 15 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya.
Bw. Masudi ametoa pongezi hizo tarehe 02.06.2025 katika kikao cha kutoa elimu kwa kamati za mradi pamoja kutambulisha mradi huo kwa wananchi, ambapo aliambatana na Wataalamu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji pamoja na wawakilishi kutoka Taasisi nyingine za Umma na kusititiza ushirikiano kutoka kwa Wananchi wakati wa Utekelezaji wa mradi huo.
Aidha wakati wa Utambulisho wa Mradi huo Kaimu Afisa Mipango Bw. Baraka Elisha amesema kuwa, Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa kiasi cha Fedha Milioni 686,135,134 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo hicho cha Afya kinachojengwa katika Kijiji cha Itebulanda zaidi ya kilomita 17 kutoka hospitali ya Wilaya.
Sambamba na hilo, Wananchi wameombwa kushiriki kikamilifu katika kuchangia nguvu kazi, kila watakapohitajika kufanya hivyo wakati wowote mpaka pale mradi utakapokamilika.
Hata hivyo, Wajumbe wa Kamati wamepewa elimu juu ya utekelezaji wa Mradi na Afisa Manunuzi wa Bw. Michael Mapela ili wautekeleze kwa kufuata sheria na miongozo ya manunuzi ili mradi utekelezeke kama ambavyo Serikali imekusudia.
Aidha Ndg. Kassumpa Machati kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) amewaasa wajumbe wa kamati kuzingatia maadili pamoja na kuepuka mianya ya Rushwa na ubadhirifu ili mradi utekelezwe kwa ubora bila kupungua kitu chochote.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Nsenda Mhe. Mahona ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mbunge Mhe. Margaret Sitta kwa kufanikisha kupatikana kwa fedha ili kujenga Kituo cha Afya katika kata ya Nsenda.
Aidha Wananchi wa Kata hiyo wamepongeza Juhudi za Diwani na Halmashauri ya Wilaya ya Urambo kwa utekelezaji wa Miradi mikubwa wanayoipata katika kata yao ya Nsenda kwani miradi hiyo italeta Manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa kata hiyo.
Kazi iendelee
Bomani Urambo
Anunani ya posta: Mkurugenzi Mtendaji (W), 30 Br ya Boma Stendi, S.L.P 170. 45582 Urambo Tabora
Simu ya mezani: +255 (0) 262 965 824
Simu ya mkononi: DED GRACE:0786821141
Barua pepe: ded@urambodc.go.tz
Copyright ©2025 Urambo . All rights reserved.