Urambo, Tabora.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Bi. Grace Quintine, leo tarehe 13.05.2025 amekabidhi jezi seti nne kwa Maafisa Elimu kutoka divisheni za Elimu ya awali na Msingi pamoja na divisheni ya Elimu Sekondari. Jezi hizo zilizoambatana na Mipira miwili, ni vifaa vilivyopatikana kupitia jitihada za dhati za Mkurugenzi Mtendaji aliyeungana na Watumishi wa Kitengo cha Utamaduni Sanaa na Michezo, Maafisa Elimu Sekondari na Msingi kwa kuchangia ununuzi wa vifaa hivyo kwa ajili ya wanafunzi watakaoshiriki UMITASHUMTA na UMISSETA 2025.
Aidha akizungumza katika tukio la utoaji wa vifaa hivyo Bi. Grace Quintine amesema kuwa, UMITASHUMTA na UMISSETA ni matukio makubwa ya Kitaifa hivyo amewasisitiza Maafisa Elimu kuendelea kufanya maandalizi yaliyo bora zaidi ili wanafunzi waweze kushiriki vyema katika michezo hiyo.Ikumbukwe kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Bi. Grace Quintine, ni mdau mkubwa wa michezo katika ngazi mbalimbali za Kitaifa, ambapo amekuwa akiunga mkono timu mbalimbali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Urambo kushiriki katika michezo mbalimbali hapa nchini. Hivyo utoaji wa jezi hizo pamoja na mipira ni muendelezo wa uungwaji mkono wa shughuli za michezo katika nyanja mbalimbali Wilayani hapa.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Jimbo la Urambo Mhe. Mrgaret Sitta ameungana na Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo na kuongeza nguvu katika maandalizi ya UMITASHUMTA na UMISSETA kwa kuchangia fedha taslimu.
Mchango wa Mbunge wa Jimbo la Urambo Mhe. Margaret Sitta kwa ajili ya wanafunzi wanaoshiriki UMITASHUMTA na UMISSETA Wilayani Urambo umewasilishwa na kupokelewa na Mkurugenzi Mtendaji kwa ajili ya kuongeza katika mahitaji ya wanamichezo. Mchango huo umewasilishwa katika ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji mnamo tarehe 13.05.2025 na Bw. Leonard Malubi - Katibu wa Mbunge kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Urambo. Mhe. Margaret Sitta ametoa fedha taslimu jumla ya Shilingi Milioni mbili (2,000,000) ambazo zitakwenda kusaidia katika maandalizi ya ushiriki wa wanamichezo hao.
Aidha siyo mara ya kwanza kwa Mbunge wa Jimbo la Urambo Mhe. Margaret Sitta kuchangia katika michezo, kwani mara kwa mara amekuwa akichangia na kuandaa mashindano mbalimbali ya kimichezo kwa ajili ya vijana na wananchi wa Urambo. Ikumbukwe kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo inaunga Mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kutia mkazo katika ukuaji wa sekta ya michezo na ukuzaji wa vipaji nchini. Hivyo kwa mwaka huu 2025 Wanafunzi watashiriki mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA.
Kazi Iendelee
Bomani Urambo
Anunani ya posta: Mkurugenzi Mtendaji (W), 30 Br ya Boma Stendi, S.L.P 170. 45582 Urambo Tabora
Simu ya mezani: +255 (0) 262 965 824
Simu ya mkononi: DED GRACE:0786821141
Barua pepe: ded@urambodc.go.tz
Copyright ©2025 Urambo . All rights reserved.