Mnamo tarehe 05.03.2025 Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji ilituma Wataalamu mbalimbali kwa ajili ya kufanya tathmini ya uharibifu na madhara yaliyowakumba wakazi wa Kata ya Kasisi, kufuatia mvua ya upepo iliyonyesha usiku wa tarehe 02.03.2025 na kupelekea kaya mbalimbali kudhurika ili kuona ni kwa namna gani wataweza kushikwa mkono. Timu hiyo iliyojumuisha Mchumi pamoja Afisa Mazingira iliweza kufika na kutembelea Kaya zilizoathirika kwa ajili ya kuona uharibifu uliotokea pamoja na kuzungumza na wahanga wa mvua hiyo ya upepo.
Akizungumza Mkuu wa Kaya moja kati ya zilizodhurika anasema ya kuwa mvua hiyo iliweza kuezua paa la nyumba yake pamoja na kudondosha sehemu ya ukuta ambao ulimuangukia mtoto wake na kumsababishia majeraha yaliyosababisha kupelekwa hospitali. Aidha ameendelea kusema kuwa kwa sasa hali ya kijana huyo siyo mbaya na ameweza kuruhusiwa kurudi nyumbani, hivyo aliiomba Serikali iweze kusaidia kaya zilizodhurika na janga la Mvua hiyo ya upepo.
Aidha akizungumzia changamto hiyo Diwani wa Kata ya Kasisi Mhe. Macho Ntayega ameeleza kuwa uharibifu uliotokea ni mkubwa katika kata hiyo ambapo Miji (Kaya) pamoja na Mazao (Mahindi pamoja na Tumbaku) vimeharibiwa katika vijiji vya kasisi pamoja na kijiji cha Mapambano. Ameeleza kuwa Kaya zilizopata madhara ni kaya 12 na kati ya hizo kaya 8 ndizo zenye madhara makubwa.
Hivyo ameiomba Serikali iweze kuwashika Mkono wananchi wa Kata ya Kasisi. Sambamba na hilo Mhe. ameziomba benki pamoja na Makampuni ya tumbaku yaweze kufanya tathmini ili yaweze kuwasaidia wakulima.
Aidha aliendelea kusema kuwa kutokana na mvua hiyo huduma muhimu ya umeme iliweza kukatwa kutokana na nguzo zaidi ya 20 kuanguka pamoja na nyaya zilizounganishwa kwenye nyumba kunyofolewa na upepo. Ameendelea kusema kuwa waliweza kuwasiliana na Shirika la TANESCO ambao walikuwa wakishughulikia madhara yaliyotokea katika njia kuu ya umeme kutoka Mkoani hivyo baada ya hapo wangeshughulikia Kata ya Kasisi, hata hivyo hadi hivi sasa Shirika la TANESCO limeweza kushughulikia changamoto hiyo ya miundombinu kwa sehemu kubwa.
Bomani Urambo
Anunani ya posta: Mkurugenzi Mtendaji (W), 30 Br ya Boma Stendi, S.L.P 170. 45582 Urambo Tabora
Simu ya mezani: +255 (0) 262 965 824
Simu ya mkononi: DED GRACE:0786821141
Barua pepe: ded@urambodc.go.tz
Copyright ©2025 Urambo . All rights reserved.