Na. Edward Rumanyika, Urambo
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilisano, Mhe. Isack Kamwelwe amezindua huduma ya mtandao wa mawasiliano ya intaneti kwa shule za Sekondari 14 zilizopo Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, ili kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa kupitia mfumo wa intaneti.
Mhe. Kamwelwe amezindua huduma hiyo Oktoba 19, 2019 katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Kutwa ya Urambo kufuatia Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom Tanzania kukubali kutoa huduma hiyo baada ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kutoa kompyuta 70 zenye thamani ya shilingi milioni 140 kwa shule hizo.
Katika kuunga juhudi za UCSAF na kufanikisha huduma za intaneti, Vodacom Tanzania imeongeza kompyuta mpakato (Laptop) 28 na vifaa vya kuwezesha kupata intaneti (routers) 14 vyenye jumla ya thamani ya shilingi milioni 68 kwa shule hizo ili wanafunzi waweze kujifunza kupitia mfumo wa TEHAMA.
Shule za Sekondari zilizonufaika na msaada huo ni Kapilula, Usisya, Imalamakoye, Chetu, Urambo, Uyumbu, Matwiga, Mukangwa, Kiloleni, Usongelani, Ukondamoyo, Ukombozi, Usoji na Vumilia.
Katika hafla hiyo, Waziri Kamwelwe ameeleza kufurahishwa na msaada ulitolewa na UCSAF na Kampuni ya Vodacom Tanzania na kusema kuwa msaada huo ni chachu ya kuendeleza jitihada za Serikali katika kukuza elimu nchini.
“Kwa niaba ya Serikali napenda kuwapongeza kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza elimu, na nitoe rai kwa Afisa Elimu Wilaya na Walimu kwa ujumla kuhakikisha vifaa hivi vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo”, alisisitiza Mhe. Kamwelwe.
Waziri Kamwelwe alitia ubani katika msaada uliotolewa kwa kuahidi kompyuta 5 kwa kwa kila shule, kwa shule tatu mpya za Sekondari Imala, Uyogo na Ugalla ambazo zimeanzishwa mwaka huu katika Wilaya ya Urambo ili nazo zisiachwe nyuma katika kutumia huduma za TEHAMA.
Alieleza kuwa mpango wa awali wa Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha shule za Sekondari 151 za umma zinaunganishwa na huduma ya intaneti kwa lengo la kuinua kiwango cha elimu.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali na wananchi wa mkoa wa Tabora, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Agrey Mwanri alisema jambo linalotendeka katika shule ya Sekondari ya kutwa ya Urambo ni kubwa na linagusa mkoa hivyo akashukuru Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote na kampuni Vodacom Tanzania kwa kurudisha sehemu ya faida yao kwa jamii na kuzitaka kampuni nyingine zinazotoa huduma katika mkoa wa Tabora kuiga mfano katika kuchangia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Afya na Elimu.
“Sisi hapa mpango tulio nao na tunaoenda nao ni kwamba kila nyumba ya Mnyamwezi itupatie graduate (mhitimu) wa chuo kikuu na ili kufikia lengo la kuwa na mhitimu wa chuo kikuu mkoa tunalenga kila mwanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita atembee na kompyuta mpakato mkononi na tutafanikiwa kwa kuunganisha nguvu zetu kama mkoa na kupitia wahisani wa maendeleo kama walivyofanya leo Vodacom Tanzania pamoja na UCSAF”, alieleza Mkuu wa Mkoa.
Awali, akisoma taarifa ya mapokezi ya kompyuta na vifaa wezeshi vya intaneti, Mkuu wa Wilaya ya Urambo Mhe. Angelina Kwingwa, alielezea changamoto zinazozikabili baadhi ya shule, zahanati na maeneo mengine ya wilaya kuwa ni kokosekana kwa nishati ya umeme na mawasiliano hafifu ya simu za mkononi na kumuomba Waziri kuyataka makampuni ya simu kujenga minara ya mawasiliano ili kungeza ufanisi wa huduma za mawasiliano.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Vodacom Foundation, Rosalynn Mworia alieleza kuwa mbali na kutoa kompyuta mpakato na vifaa vya intaneti kampuni hiyo pia inalengo la kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa walimu wawili kutoka kila shule iliyonufaika na vifaa hivyo ili kuwajengea uwezo wa kuvitumia wakati wa kujifunza na kufundisha.
Pia vodacom wametoa tovuti (instant schools.vodacom.co.tz) yenye maudhui ya elimu inayopatikana bure kupitia vodacom kwa lengo la kumsaidia mwalimu na mwanafunzi kupakua vitabu mbalimbali, nukuu za masomo, rejea za mitihani ya miaka ya nyuma ili waweze kujisomea kupitia huduma ya TEHAMA.
-Mwisho-
Bomani Urambo
Anunani ya posta: Mkurugenzi Mtendaji (W), 30 Br ya Boma Stendi, S.L.P 170. 45582 Urambo Tabora
Simu ya mezani: +255 (0) 262 965 824
Simu ya mkononi: DED GRACE:0786821141
Barua pepe: ded@urambodc.go.tz
Copyright ©2025 Urambo . All rights reserved.