Jamii imetakiwa kushirikiana katika malezi na makuzi ya mtoto tangu anapokuwa tumboni hadi kuzaliwa kwake, kwani ukuaji wa mtoto hutegemea zaidi kusikia na kuona.
Hayo yamesemwa na Afisa Ustawi wa jamii Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Bw. Paul Kahumbi wakati akitoa elimu kwa wazazi katika kilele cha Siku ya Familia Duniani inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo Mei 15 na mwaka huu wa 2024 madhimisho hayo ngazi ya wilaya yamefanyika katika Kijiji cha Igunguli Kata ya Uyogo na kauli Mbiu ilikuwa “TUKUBALI TOFAUTI ZETU KWENYE FAMILIA, KUIMARISHA MALEZI YA WATOTO”.
Mgeni Rasmi alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Urambo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi (SACC) Elibariki Bajuta.
Pamoja na Mgeni Rasmi Sherehe hii ilihudhuriwa na wageni mbalimbali ambao ni Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Urambo, Diwani wa kata yaUyogo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Bi. Grace Quintine akiambatana na timu ya Wakuu wa Idara, Watumishi mbalimbali kutoka taasisi tofauti, Uongozi wa kijiji pamoja na wadau wengine kutoka kwenye Mashirika yasiyo ya Kiserikali.
Aidha Bw. Paul Kahumbi alisema mtoto anahitaji malezi ya Baba na Mama tangu akiwa Tumboni kwani wakati huo ndio wakati ambao mtoto husikia zaidi yale yanayotendeka akiwa Tumboni mwa mama yake. Aliendelea kwa kuwahimizi akina baba kuishi vizuri na wenza wao zaidi katika kipindi hicho kuepusha wenza wao kupata msongo wa mawazo unaoweza kuathiri ukuaji wa mtoto aliye tumboni kwani mtoto anapozaliwa huwa na ukuaji wa ubongo wa 25% na mtoto atakayelelewa vizuri ubongo wake hufikia 80% pale anapofikisha miaka 3, hivyo malezi ya mtoto hutegemea zaidi miaka 0-3.
Hata hivyo Afisa Ustawi wa Jamii alieleza kuwa ubongo wa mtoto anapozaliwa hadi kufikia miaka 3 hupokea mambo mengi. Mtoto anapofikisha miaka 4 ubongo hufanya Usafi na kubakiza vitu vya msingi alivyopokea kwenye 0-3. Hivyo wazazi huamua wenyewe kuwa na mtoto mwenye uwezo mkubwa au mdogo kiakili kutokana na malezi aliyoyapata kwenye miaka 0-3. Aidha aliwaasa wazazi kuwashauri na kuwalea watoto vyema ili kuwa na watoto wenye tabia njema kwani tabia za binadamu huchangiwa na malezi aliyoyapata kutoka 0 hadi 3.
Sambamba na hilo mwakilishi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) Ndg. Alfred Kalugendo alisema Ukatili wa kijinsia upo kwa kiwango kikubwa na kuna makundi mawili makubwa ambayo ni Wanawake na Watoto ndio wahanga wakubwa wa matukio ya ukatili wa kijinsia. Aidha Ndg Kalugendo alisema ukatili unaweza kufanyika sehemu yoyote na ukatili huwa kwa namna mbalimbali ikiwemo kijinsia, kimwili, kisaikolojia, kiuchumi, kiafya, kielimu n.k hivyo kuwaasa wananchi kupiga vita Ukatili wa Kijinsia na kuhakikisha katika familia na kijamii Mtoto anapewa kipaumbele “Mtoto Kwanza”.
Aidha Mkuu wa Kituo cha Polisi wilaya ya Urambo ACP. Mwalukasa alieleza kuwa ili kuupiga vita ukatili wa kijisia jamii inapaswa kujali zaidi malezi ya watoto na kuwa makini na mabadiliko wanayopitia watoto wao. Pia alisisitiza usawa wa ugawaji wa majukumu na malezi kwa watoto kwani husaidia kuboresha saikolojia ya watoto katika kufikia ndoto zao na kuzijua nafasi zao katika jamii hivyo sote tuupige vita mfumo dume na Mila potofu katika jamii .
Aidha ACP. Mwalukasa aliendelea kusisitiza jamii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na vyombo vya ulinzi na usalama kwa pamoja wanapaswa kusimamia uwajibikaji kwani kesi nyingi za ukatili wa kijinsia hazifiki mwisho kutokana na sababu mbalimbali kama wananchi wenyewe kukataa kutoa ushirikiano, hivyo wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano kwa wadau mbalimbali na vyombo vya ulinzi na usalama ili adhabu zitolewe kwani kuendekeza matukio ya ukatili hupelekea watoto kuiga na kuyatekeleza wanapokuwa wakubwa.
Sambamba na hilo ACP. Mwalukasa alisema wazazi kuishi na watoto vizuri ili watoto waweze kuwaeleza yale wanayopitia shuleni na kwenye jamii kwa ujumla, kwani kwa hali hiyo husaidia kugundua mapema kama mtoto anapitia ukatili wa aina yoyote ile. Aliongeza kwa kusema, pamoja na juhudi zote hizo, Kila mmoja kwa imani yake amshirikishe Mwenyezi Mungu kwa kumuomba kuwasimamia, kuwabariki na kuwalinda watoto wetu.
Aidha Mgeni rasmi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Elibariki Bajuta aliwaasa wananchi waliohudhuria sherehe ya siku ya Familia duniani kuwapa watoto malezi mema, kuwafuatilia na kuwakanya kutembea usiku na kupokea vizawadi na vitu vinginevyo kutoka kwa watu wanaowarubuni. Pia wazazi kuhakikisha watoto wao wanaenda shule na kurudi nyumbani kwa wakati na kufuatilia kwa ukaribu malezi yao wakiwa shuleni na nyumbani.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Urambo SACC Bajuta aliwataka wazazi kuwapeleka watoto wao shule na kuacha kuwatumia watoto katika shughuli za kiuchumi kwani ni Kinyume cha Sheria na yeyote atakayegundulika kukataa kupeleka mtoto shule au kumtumia mtoto katika shughuli za kiuchumi atapata adhabu kali kwa mujibu wa Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
SACC Bajuta aliwasisitiza wazazi kuepuka kuwaruhusu watoto kwenda katika maeneo hatarishi yanayowea kuhatarisha usalama wao kama kwenye maji yenye kina kirefu. Pamoja na Hayo amewaasa wazazi kuyafanyia kazi yale yote waliyoelezwa na wataalamu kwani kiwango cha ukatili wa kijinsia katika Wilaya ya Urambo ni mkubwa sababu iliyopelekea wataalamu kufika na kutoa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia.
Smbamba na hilo Mkuu wa Wilaya ya Urambo SACC Elibariki Bajuta, Aliwapongeza wananchi wa Kata ya Uyogo kwa juhudi zao katika kilimo hasa kilimo cha Tumbaku na kuwaasa kuacha kutorosha Tumbaku na kuwa walinzi wa wengine ili wasitoroshe Tumbaku kwani kwa kutorosha Tumbaku ni kuinyima mapato Halmashauri ya Wilaya ya Urambo na kuwapa mzigo wa madeni wakulima wengine kwenye vikundi vyao vya mikopo.
Aidha SACC Bajuta alimalizia kwa kusema Msimu ujao wana Igunguli waendelee kufanya vizuri zaidi katika kilimo na kuwaeleza kuwa Msimu ujao Mkulima ataweza kukopa mwenyewe kwenye vyama vya Msingi vya Tumbaku (AMCOS) na kufanya kilimo chake. Utaratibu huu umekuja ili kudhibiti utoroshaji wa Tumbaku unaoacha Mzigo wa madeni kwenye vikundi kwa Wale wasiotorosha.
Bomani Urambo
Anunani ya posta: Mkurugenzi Mtendaji (W), 30 Br ya Boma Stendi, S.L.P 170. 45582 Urambo Tabora
Simu ya mezani: +255 (0) 262 965 824
Simu ya mkononi: DED GRACE:0786821141
Barua pepe: ded@urambodc.go.tz
Copyright ©2025 Urambo . All rights reserved.