Wilaya ya Urambo imegawa madawati 819 ikiwa ni awamu a Pili katika shule 13 kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madawati na kuboresha sekta ya elimu.
Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa madawati hayo, Mkurugenzi Mtendaji amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo inatekeleza dhima ya Serikali kwa kuhakikisha wanafunzi katika shule zote za msingi na sekondari wanakaa kwenye madawati.
Na katika kuhakikisha hilo linatimia, tarehe 19.08.2024 Wilaya ya Urambo imegawa madawati 819 katika shule 13 ili kupunguza uhaba wa madawati katika shule hizo.
Akizungumzia kuhusu kampeni ya kumaliza tatizo la uhaba wa madawati Urambo, Bi. Grace Quintine amesema kuwa Wilaya ya Urambo ilianzisha kampeni ya kutengeneza madawati baada ya kubaini uwepo wa upungufu wa madawati 7,225 kwa shule za msingi na viti na meza 649 kwa shule za sekondari. Hivyo Mhe Mkuu wa Wilaya aliyekuwepo wakati huo SACC. Elibariki Bajuta kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya aliamua kuanzisha kamopeni hiyo kupitia kauli mbiu isemayo "Dawati ni Elimu, Kukaa chini Urambo sasa basi" na kufanikiwa kugawa madawati 1,584 Katika awamu ya Kwanza na awamu hii ya pili madawati 819 na kufanya jumla ya madawati yaliyogawiwa kufikia 2,403.
Madawati hayo 819 yametoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Urambo kwa mchanganuo ufuatao JTI madawati 300, Halmashauri ya Wilaya madawati 137, HALEM Construction madawati 14, Gereza la Kilimo madawati 10 pamoja na michango ya wadau mbalimbali yenye jumla ya madawati 358 hivyo kufanya jumla ya madawati yote kuwa 819.
Mkurugenzi Quintine amesema pamoja na kutengeneza asilimia kubwa ya madawati hayo kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri, amewashukuru wadau wa maendeleo waliofanikisha kupatikana kwa madawati mengine mengi katika awamu zote mbili na kusaidia kupunguza tatizo la uhaba wa madawati Urambo.
Hata hivyo Bi. Grace Quintine amesema kwa hatua hii ya mwanzo wameanza na shule zenye uhitaji wa haraka na wataendelea kugawa madawati kadiri yanavyotoka katika Vituo ambavyo vinatengeneza lengo ni kila shule ipate madawati ya kutosha.
Aidha Mkurugenzi Quintine amewahimiza Wanaurambo kuwa watoto wapelekwe shule kwani Serikali imeandaa mazingira mazuri, na wakati huu Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za Msingi mbili (02) na Sekondari mbili (02) Wilayani Urambo ambapo mpaka Januari 2025 shule zitakuwa tayari ili kuweza kupokea wanafunzi wapya.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Urambo Mhe. Dkt. Khamis Athumani Mkanachi baada ya kupokea taarifa hiyo amepongeza jitihada za mtangulizi wake SACC. Elibariki Simon Bajuta kwa juhudi zake katika kuanzisha kampeni hiyo ambapo hadi sasa madawati hayo yanaendelea kutengenezwa na kuweza kugawiwa kwenye shule mbalimbali kwa ajili ya kupunguza uhaba wa madawati. Hata hivyo Dkt. Mkanachi amesisitiza kuwa ataendeleza yale yote mazuri yaliyoanzishwa na watangulizi wake ili Urambo izidi kusonga mbele.
"Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, jitokeza kushiriki Uchaguzi"
Bomani Urambo
Anunani ya posta: Mkurugenzi Mtendaji (W), 30 Br ya Boma Stendi, S.L.P 170. 45582 Urambo Tabora
Simu ya mezani: +255 (0) 262 965 824
Simu ya mkononi: DED GRACE:0786821141
Barua pepe: ded@urambodc.go.tz
Copyright ©2025 Urambo . All rights reserved.