“Niwaombe sana Muilinde Miradi hii ya Maji, Serikali inatumia Fedha nyingi kuleta Mradi Mkubwa kama huu wa maji” Maneno hayo yamezungumzwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Paul Matiko Chacha alipotembelea Wilaya ya Urambo kwa ajili ya kufanya Ziara pamoja na Uzinduzi wa Miradi ya Maji.
Mkuu wa mkoa ametembelea mradi wa Bwawa la maji la Kalemela A ambapo amepewa taarifa ya Mradi kutoka kwa Meneja wa Ruwasa Wilayani Urambo Ndg. Gendai ambaye ameeleza kuwa mradi huo umegharimu Zaidi ya bilioni 5 na unatarajia kuhudumia wananchi wa Vijiji 17 katika Wilaya ya Urambo ambao ni Zaidi ya wananchi 148,000 na hali ya Mradi kwa sasa ni asilimia 55. Aidha ndg. Gendai amemueleza Mkuu wa Mkoa hatua zote walizopitia katika ujenzi wa Mradi huo.
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Paul Chacha, amewapongeza RUWASA kwa juhudi wanazozifanya katika kutatua kero ya maji kwa wananchi wa Wilaya ya Urambo na anaona kufikia mwisho wa mwaka huu tatizo la maji Urambo litaweza kupungua kwa kiasi kikubwa.
Aidha wananchi wa Kijiji cha Kalemela “A” Wameshukuru uongozi wa Wilaya, Mkoa pamoja na Mhe. Rais kwa juhudi wanazozifanya kuhakikisha maendeleo yanapatikana Urambo hasa kwa kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na Salama kwa ajili ya matumizi ya Binadamu.
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Tabora aliweza kuzindua Mradi wa maji katika kijiji cha Ifuta ambao umekamilika na Wananchi wameanza kupata huduma katika mradi huo. Mradi wa maji katika Kijiji cha Ifuta una thamani ya zaidi ya milioni 300 na ni moja kati ya Miradi ya kisasa uliojengwa kwa maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo wananchi huchota maji kwa kutumia kadi zao.
Aidha Mhe. Mkuu wa mkoa wa Tabora pamoja na Uongozi wa Wilaya ulishuhudia Makabidhiano ya mradi huo kutoka katika upande wa RUWASA kwenda kwa mamlaka ya kijiji cha Ifuta.
Sambamba na hilo, Mhe. Paul Chaha amesisitiza wananchi kuepuka ukatili kwa Watoto na kuacha Watoto wasome. Aliendelea kusisitiza kuwa , katika jamii inapobainika kuna mtu anafanya Vitendo hivyo afikishwe kwenye vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Paul Matiko Chacha amewasisitiza wananchi kujitokeza kwa Wingi katika zoezi la kuboresha daftari la kudumu la Wapiga Kura kwani ni haki ya kila Mtanzania mwenye vigezo vya kupiga kura kushiriki.
Aidha wananchi wa kijiji cha Ifuta wamemshukuru Mhe. Rais kwa juhudi zake za kumtua mama ndoo kichwani kwani kupitia Mradi huo wa maji, Wakazi wa Kijiji cha Ifuta wananufaika na kuacha kutembea umbali mrefu kufuata maji pamoja na kutumia maji yasiyo safi na Salama.
Bomani Urambo
Anunani ya posta: Mkurugenzi Mtendaji (W), 30 Br ya Boma Stendi, S.L.P 170. 45582 Urambo Tabora
Simu ya mezani: +255 (0) 262 965 824
Simu ya mkononi: DED GRACE:0786821141
Barua pepe: ded@urambodc.go.tz
Copyright ©2024 Urambo . All rights reserved.