Na. Edward C.Rumanyika, Urambo
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu amepiga goti kama ishara ya kuwashukuru wananchi wa Kijiji cha Uhuru, Kata ya Vumilia Wilayani Urambo mkoani Tabora, baada ya wananchi hao kutoa eneo la ekari tano bure kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kupoozea umeme.
Naibu Waziri Mgalu alitoa shukrani hizo kwa wananchi Jumatano Julai 17, 2019 na kuupongeza uongozi wa Kijiji cha Uhuru na kueleza kuwa kukamilika kwa ujenzi kituo cha kupoza umeme kitakachojengwa katika eneo walilolitoa ifikapo mwezi Agosti mwaka 2020, kutaondoa adha ya kukatika kwa umeme katika Wilaya za Urambo, Uyui na Kaliua.
"Wananchi wa kijiji cha Uhuru mmekuwa watu wa pekee kwa kutoa ardhi yenu kutuwezesha kujenga kituo hiki bila ya kudai fidia, na sisi Serikali ya Awamu ya Tano tunatambua mchango wenu mkubwa tunapoelekea katika uchumi wa viwanda hivyo nasema ahsenteni," aliwashukuru wananchi huku akiwa amepiga magoti mbele ya umati wa wananchi.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo ,Mhandisi wa Mradi huo Julius Kabengwe, alisema kuwa mradi utagharimu shilingi 1, 160,429,066 kwa awamu ya kwanza na mradi utatekeleza kazi za ujenzi wa uzio, ofisi za kuendeshea kituo, barabara ya kuingia kituoni toka barabara ya Urambo-Kaliua, ununuzi na ufungaji wa transifoma kubwa mbili zenye uwezo wa 10 MVA kila moja na ujenzi wa laini ya msongo wa kilovoti 132kV kutoka Tabora mjini hadi Uhuru-Urambo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mgalu alizindua umeme wa mradi wa REA Awamu ya III Mzunguko wa Kwanza-Urambo, wenye urefu wa kilometa mbili unaotekelezwa katika kata ya Kasisi kijiji cha Wema.
Akihutumia wananchi, viongozi wa Serikali na Chama, Naibu Waziri aliuagiza uongozi wa TANESCO-Urambo na REA-Urambo kuhakikisha mitaa 13 iliyoko Urambo inasambaziwa umeme na kuwafungia wananchi kwa bei isiyozidi shilingi 27,000 na kumtaka mkandarasi wa mradi wa REA awamu ya III mzunguko wa Kwanza kuhakikisha vijiji saba vilivyo salia vinasambaziwa umeme katika REA Awamu ya III mzunguko wa Pili ili kuifaya wilaya ya Urambo kuwa mingoni mwa wilaya zenye umeme kila kijiji.
Aidha, Mhe. Magalu alizisisitiza TANESCO na REA pia kupeleka umeme katika taasisi mbalimbali zikiwemo nyumba za ibada, vituo vya umma na binafsi vya kutolea huduma na akasisitiza kuhakikisha kila nyumba inayostahili kuwekewa umeme iwekewe bila kujali kama nyumba hiyo niya udongo au tofali.
Kwa upande wake, Bi. Yulitha Misalaba ambaye nyumba yake ilifanyiwa uzinduzi kwa kuwashwa umeme, alimshukuru Naibu Waziri na Mbunge wa Urambo Mhe. Magreti Simwanza Sitta kwa juhudi zake za kuhakikisha anatimiza ahadi alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2015.
"Nafuhi sana kwani na sisi tutakuwa kama wa mjini, kwani tulikuwa tunahangaika sehemu za kuchajia simu zetu, yaani ahasante sana Mbunge wetu, ahasante Magufuli", alieleza kwa furaha Bi. Misalaba.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Diwani wa Kata ya Kasisi, Mhe. Japhet Kakumbi alielezea kufurahishwa na mradi wa REA Awamu ya III mzunguko wa Kwanza kuanzia katika Kata anayoiongoza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri ya kuwaletea wananchi wake maendeleo na kuwaomba wananchi kutumia umeme huo kama fulsa kwa kuanzisha biashara mbalimbali zikiwemo saluni za kike na kiume, mashine za umeme za kusaga na kukoboa nafaka na kuwataka wanafunzi watumia umeme huo kusoma na kujifunzia.
Bomani Urambo
Anunani ya posta: Mkurugenzi Mtendaji (W), 30 Br ya Boma Stendi, S.L.P 170. 45582 Urambo Tabora
Simu ya mezani: +255 (0) 262 965 824
Simu ya mkononi: DED GRACE:0786821141
Barua pepe: ded@urambodc.go.tz
Copyright ©2024 Urambo . All rights reserved.