Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Urambo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Elibariki Bajuta amefanya makabidhiano ya ofisi kwa Mkuu wa Wilaya ya Urambo aliyeteuliwa hivi karibuni Dkt. Khamis Athumani Mkanachi. Zoezi hilo limefanyika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya na kumaliziwa na hafla ya Kumuaga SACC Elibariki Bajuta na kumkaribisha Dkt. Khamis Athumani Mkanachi.
Sambamba na tukio hilo la makabidhiano ya ofisi, Watumishi wa Halmashauri ya Urambo, madiwani, wafanyabiashara, Watumishi kutoka Taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali pamoja na wadau mbalimbali walijumuika pamoja katika Hafla maalumu ya kumuaga aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Urambo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Elibariki Bajuta na kumkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Urambo Dkt. Khamis Athumani Mkanachi.
Aidha katika hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Bi. Grace Quintine kwa niaba ya Watumishi amemshukuru SACC Bajuta kwa muda wote aliokuwepo katika Wilaya ya Urambo kwani ameisaidia sana kati shughuli mbali mbali hasa Miradi ya Maendeleo na ukusanyaji wa mapato. Bi. Quintine ameendelea kusema kuwa anamtakia maisha mema na nafasi ya juu zaidi kwani Mhe. Rais atampangia majukumu mengine.
Aidha, SACC Bajuta amewashukuru wote kwa namna ambavyo walishirikiana naye katika shughuli mbalimbali wakati wa utumishi wake kama Mkuu wa Wilaya ya Urambo na kusisitiza kuwa ushirikiano ambao wameutoa kwake wautoe pia kwa Mkuu mpya wa Wilaya. SACC Bajuta amewashukuru kwa kipekee watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo kwa kushirikiana naye katika shughuli mbalimbali.
Mkuu mpya wa Wilaya ya Urambo Dkt. Khamis Athumani Mkanachi amewashukuru watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo kwa mapokezi aliyoyapata na kuwashukuru wote waliohudhuria katika hafla hiyo kwa ajili ya kumuaga SACC. Bajuta na kumkaribisha yeye. Aidha amemuahidi SACC Bajuta kuwa atayaishi yote mazuri aliyoyafanya kwa ajili ya Wanaurambo. Dkt. Mkanachi ameomba ushirikiano ili kuweza kusukuma gurudumu la maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Urambo.
Aidha watumishi na wadau mbalimbali waliweza kuzungumza ni kwa namna gani walimfahamu SACC. Bajuta na kufanya naye kazi, ambapo wengi walimtaja kama mchapakazi, msikivu na mtenda haki huku wakitamani afike mbali zaidi ya nafasi aliyokuwa nayo.
Bomani Urambo
Anunani ya posta: Mkurugenzi Mtendaji (W), 30 Br ya Boma Stendi, S.L.P 170. 45582 Urambo Tabora
Simu ya mezani: +255 (0) 262 965 824
Simu ya mkononi: DED GRACE:0786821141
Barua pepe: ded@urambodc.go.tz
Copyright ©2024 Urambo . All rights reserved.