Mwalimu ni mtu muhimu na mwenye thamani kubwa hapa nchini kwani hufanya mengi na Taifa linawategemea. Hiyo ndiyo sababu hata Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere enzi za uhai wake, hakuwahi kufuta jila la “Mwalimu” katika utambulisho wake.
Maneno hayo yamezungumzwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) Dkt. Charles Msonde katika mkutano maalumu alioufanya na Watumishi wa Kada ya Ualimu kwa Shule za Msingi na Sekondari Wilayani Urambo tarehe 09.06.2024 karika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Margareth Sitta.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi, amefanya Mkutano huo kwa lengo la kuzungumza mambo mbalimbali yanayogusa sekta ya Elimu akiwa ameambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Bi. Grace Quintine ambaye aliongozana na timu ya wataalamu mbalimbali kutoka Idara ya Utawala pamoja na Elimu Msingi na Sekondari. Aidha, Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Mbunge wa Jimbo la Urambo Mhe. Margareth Sitta. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa vyama vya Walimu kwa ngazi ya Wilaya na Mkoa wa Tabora.
Aidha, Dkt. Msonde amesema yeye ni mtumishi na yupo kwa ajili ya kuwatumikia watu na hivyo kama kuna changamoto ambazo waalimu hupitia ni vyema aambiwe, kwani kupitia wengine waliowahi kueleza changamoto zao walifanikiwa kufahamu changamoto kuu sita ambazo zina wasumbua Walimu. Jambo la kheri ni kwamba changamoto zote Sita tayari zimekwishatatuliwa kwa maslahi ya walimu wote nchini.
Dkt Msonde aliendelea kusema kuwa, baadhi ya Changamoto hizo ni upandaji wa madaraja na vyeo, Malipo ya Likizo na Uhamisho, Malimbikizo ya mishahara Pamoja na Kauli mbaya wanazokumbana nazo Walimu. Katika kuzungumzia changamoto hizo, Dkt. Msonde amesema kama Ofisi wameweza kupitia madaraja ya Walimu ili kuona ni yupi anastahili kupanda daraja na vyeo na wamefanikiwa kupata walimu zaidi ya 50,000 ambao wanapaswa kupanda vyeo na kwa urambo wapo wanaostahili.
Sambamba na hilo Dkt. Msonde amesema kwa kushirikiana na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI na Mhe. George Boniface Simbachawene ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wameweza kutatua Changamoto nyingi ikiwemo malipo ya Malimbikizo ya mishahara kwa Walimu. Hata hivyo amesema endapo kama wapo wenye changamoto hiyo kwa Wilaya ya Urambo, wapeleke viambata vyao na kuviwasilisha kwa Afisa Elimu naye aende kwa Afisa utumishi kwa ajili ya kushughulikia changamoto hiyo. Endapo kutakuwa na mkwamo, wasisite kufikisha changamoto zao kwa Mkurugenzi Mtendaji.
Aidha Naibu katibu mkuu OR-TAMISEMI amewasisitiza Walimu kuzingatia ufundishaji wa malengo, mbinu na mikakati huku wakipaswa kuepuka ufundishaji wa mazoea ili kusaidia kuinua ufaulu kwa wanafunzi. Hata hivyo Dkt. Msonde amesisitiza Walimu kuzingatia kufundisha zaidi Lugha ya Kiingereza, ambapo mwanafunzi akifahamu lugha, uwezo wa kuelewa na kujibu maswali huwa mkubwa Zaidi kwani mifumo ya uulizwaji maswali huhitaji uelewa Zaidi.
Aidha, katika mkutano huo, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Bi. Grace Quintine amemshukuru mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha miundombinu ya sekta ya Elimu hasa katika Wilaya ya Urambo ambapo kupitia fedha zinazotoka Serikali kuu pamoja na mapato ya ndani imesaidia kuongeza matundu ya vyoo, madarasa na miundombinu mingine mingi katika sekta ya Elimu. Aidha Urambo inapambana kuhakikisha chakula kinapatikana shuleni na wanafunzi wanapata Mlo ambao una virutubisho, hivyo halmashauri inategemea katika viashiria vya lishe kufanya vizuri. Ameendelea kusema kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Sita anaamini ujio wa Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI utakuwa na tija katika kusaidia kuinua sekta ya Elimu Wilayani Urambo.
Sambamba na hilo Mkurugenzi Quintine, amemshukuru Mbunge wa Urambo Mama Margareth Sitta kwa upendo wake kwa Wananchi wa Wilaya ya Urambo, kwani kupitia yeye ameendelea kuhakikisha anatafuta wadau wa maendeleo na kushirikiana nao katika kuboresha Urambo, pia leo tunayo shule ya Margareth Sitta ambayo ni shule nzuri na yenye miundombinu bora kwa ajili ya wanafunzi wa Tanzania nzima. Mkurugenzi Quintine ameendelea kwa kusema kuwa upendo wa Mama Margareth Sitta haupimiki, kwani angeweza kuendelea na shughuli nyingine lakini ameamua kubaki Urambo na kujumuika na walimu na wananchi katika mambo mbalimbali.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Bi. Grace Quintine amesema kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Urambo ina mkakati wa kupunguza tatizo la upungufu wa madawati shuleni na pia ina mpango wa kuinua ufaulu katika Shule zake. Amesema kwa sasa wameweka nia Madhubuti ya kuhakikisha ufaulu unapanda kwa Wanafunzi wa Wilaya ya Urambo. Mafanikio haya yanahitaji Zaidi juhudi za Walimu, kwani walimu ni wa thamani na Taifa linawategemea.
Bomani Urambo
Anunani ya posta: Mkurugenzi Mtendaji (W), 30 Br ya Boma Stendi, S.L.P 170. 45582 Urambo Tabora
Simu ya mezani: +255 (0) 262 965 824
Simu ya mkononi: DED GRACE:0786821141
Barua pepe: ded@urambodc.go.tz
Copyright ©2024 Urambo . All rights reserved.