"Kwa Mtazamo wangu kama Msimamizi wa Serikali katika Wilaya ya Urambo, kufikia mwezi Novemba hali ya Upatikanaji wa maji, nina imani itakuwa zaidi ya 70% mpaka 75% kwa sababu Kasi ya miradi ni kubwa"
Maneno hayo yalizingumzwa na Mkuu wa Wilaya ya Urambo Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Elibariki Bajuta alipotembelea na kuzindua Miradi miwili ya kisasa ya maji katika kijiji cha Nsogolo kata ya Uyumbu na kijiji cha Mtakuja kata ya Nsenda ikiwa ni katika kutekeleza agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyeagiza wananchi watengenezewe utaratibu wa kutumia maji kulingana na fedha walizonazo.
Mkuu wa Wilaya ya Urambo aliambatana na Kamati ya Usalama, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Mhe. Adam Malunkwi, Timu ya wajumbe kutoka Chama Cha Mapinduzi Wilayani Urambo wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Urambo Ndg. Shabani Mussa na Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilayani Urambo pamoja na wataalamu kutoka RUWASA. Aliambatana pia na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Urambo ambao waliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Bi. Grace Quintine.
Miradi hiyo ya maji iliyojengwa kupitia RUWASA kwa fedha kutoka Serikali kuu inayogharimu Tsh 130,569,930/= kwa kila Mradi imesaidia wananchi kupata huduma ya maji safi na salama ambapo kwa kijiji cha Nsogolo Mradi unatarajiwa kuhudumia wakazi zaidi ya 2000 na wakazi wengine wengi katika kijiji cha Mtakuja.
Aidha wananchi wamemshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama kulingana na kiasi alichonacho mtu. Kwani kabla ya kutekelezwa miradi hiyo ya maji wananchi walikuwa wakitegemea kupata maji kutoka katika visima vifupi ambavyo havikuwa na maji safi na salama na wengi walikumbana na changamoto za kupata maradhi kutokana na maji hayo.
Baada ya uzinduzi huo Meneja wa RUWASA Wilayani Urambo Mhandisi Gendai, alikabidhi Miradi hiyo na kutia saini makubaliano kati ya RUWASA na vyombo vya Community Based Water Supply Organization (CBWSO) kwa kila eneo husika.
"Hali ya maji katika Wilaya ya Urambo ni kama 50% ya upatikanaji wa maji, Na mpango wa Serikali ni kuhakikisha ndani ya Mwaka huu na mwaka ujao hali ya upatikanaji wa maji kufikia Asilimia 100" DC Bajuta.
Aidha ameendelea kusema Utekelezaji wa mpango huo unaendelea kwa kasi kwani Serikali inatekeleza miradi Mikubwa Miwili ya kimkakati ambao ni Mradi wa maji ya Ziwa Victoria unaotoka Tabora kuja Urambo. Mradi huu unatekelezwa kwa pamoja katika Wilaya ya Sikonge Kaliua na Urambo. Na jambo jema ni kuwa Utekelezaji wa Mradi huo tayari upo ndani ya Wilaya ya Urambo na unaendelea vizuri kwa ngazi ya Uchimbaji na ulazaji wa mabomba pamoja na Ujenzi wa Matanki ya kuhifadhia maji kwa ajili ya kusambaza maji kwa wananchi.
Urambo tumejengewa matanki mawili makubwa katika kata ya Muungano yenye ujazo wa Lita Milioni mbili kwa kila Tanki moja. Na Tanki moja litatumika kwa Wilaya ya Urambo na La pili kwa Wilaya ya Kaliua. Mradi huu unatumia fedha nyingi zaidi ya Bilioni 150, hivyo anaishukuru Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha Wananchi wa Urambo wanapata Maji safi na Salama na Miradi kukamilika kwa wakati. Pamoja na mradi kupungua kasi kutokana na Mvua, hivi sasa Mkandarasi anaendelea na kazi kwa kasi.
Pia Mradi wa pili ni wa Bwawa la maji katika kijiji cha Kalemela "A" kata ya Muungano unaogharimu zaidi ya Bilioni 5.9 unaotarajiwa kuhudumia vijiji 17 na wananchi zaidi ya 148,000. Mradi huo wa Bwawa unaendelea kwa kasi na umefikia Utekelezaji wa 53%, inatarajiwa kufikia mwezi Novemba Mkandarasi atakabidi Mradi kwa Serikali ili ukabidhiwe kwa Wananchi. Hivyo Serikali inafanya kazi kwa kasi kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na Salama.
Aidha katika kijiji cha Usoke Mjini Mradi mwingine unatekelezwa wenye thamani ya Tsh 973,677,559/= kwa fedha kutoka Serikali kuu na hali ya mradi mpaka sasa imefikia 58%. Kukamilika kwa Mradi huu kutasaidia upatikanaji wa Maji safi na salama kwa wananchi zaidi ya 4000 katika kijiji cha Ussoke Mjini pamoja na Ussoke Mlimani.
SACC. Bajuta alisema kuna Mradi mwingine wa Visima 12 kwenye kata ya Nsenda, Ukondamoyo na Songambele unaogharimu zaidi yaTsh 601,000,000/= Pia upo Mradi mwingine wa Visima 6 unaogharimu zaidi ya Tsh 220,000,000/=
Sambamba na hilo upo Mradi mwingine unaotekelezwa katika maeneo ya upatikanaji wa huduma za Afya ambapo kuna Vituo vya Afya viwili vipya vinavyotarajiwa kufunguliwa hivi karibuni ambavyo ni Kituo cha Afya cha Ussoke Mlimani na Kituo cha Afya cha Vumilia ambapo RUWASA wameweka fedha zaidi ya Tsh 300,000,000/= kuhakikisha maji yanapatikana katika Vituo hivyo vya Afya.
Aidha upo Mradi Mwingine unaotekelezwa katika Kijiji cha Sipungu wenye zaidi ya Tsh 900,000,000/= ambao kazi imeanza.
Amesisitiza wananchi wa Urambo kuwa na imani na Serikali ambayo ina Mkakati mkubwa sana wa kuhakikisha wanapata Maji safi na Salama. SACC. Bajuta ameishukuru Serikali kwa kuitengea RUWASA Wilaya ya Urambo Bilioni 4.2 kwa ajili ya Kutekeleza Miradi katika Wilaya ya Urambo. Kwani Fedha hizi pamoja na Miradi mingine ni nyingi sana na zimeletwa kwa Sababu Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anawapenda sana Wananchi wa Urambo, hivyo wananchi wazidi kuwa na imani na Serikali ya Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Aidha ametoa Rai kwa Wananchi kutunza miundombinu ya maji kwani ni mali ya kila mwananchi, hivyo siyo jambo jema kuharibu miradi kwani Serikali imetumia fedha nyingi kuijenga. aidha SACC. Bajuta amemsisitiza Diwani kupita katika kila kijiji kuwaeleza wananchi Serikali imefanya kazi gani, kwani wasiposikia kutoka kwa viongozi na wataalamu, watasikia kutoka kwa watu wengine na watapotoshwa.
Kazi inayofanywa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inaonekana hivyo aliwahakikishia wananchi aa Mtakuja kuwa barabara zote zilizoharibiwa na Mvua zitarekebishwa Kwani TARURA wamejipanga na katika maeneo mengi ya Wilaya ya Urambo wakandarasi wapo kazini kwa kasi kuhakikisha barabara zinakamilika. Katika Kata ya Kiloleni Mkandarasi anaendelea na kazi, kata ya Ukondamoyo barabara imekamilika na Kata ya Nsenda mkandarasi atafika. Hivyo Bbarabara zenye changamoto katika maeneo yote zitakwenda kukarabatiwa.
Bomani Urambo
Anunani ya posta: Mkurugenzi Mtendaji (W), 30 Br ya Boma Stendi, S.L.P 170. 45582 Urambo Tabora
Simu ya mezani: +255 (0) 262 965 824
Simu ya mkononi: DED GRACE:0786821141
Barua pepe: ded@urambodc.go.tz
Copyright ©2024 Urambo . All rights reserved.